Pia imewataka wamiliki wa maeneo ya burudani, starehe na nyumba za ibada kuzingatia matumizi ya vipima kelele na vizuia sauti ili kuhakikisha jamii zinazozunguuka maeneo hayo haziathiriwa na kelele wanazozisababisha.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Selemani Jafo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 03, 2023 jijini Dodoma.
"Kanuni za udhibiti wa kelele na mitetemo za mwaka 2015, zimeainisha viwango vya sauti vinavyoruhusiwa kwenye maeneo ya makazi, biashara, viwanda na hospitali ili kulinda afya ya jamii hivyo, nitoe wito kwa wananchi kutoa taarifa kuhusu kelele na mitetemo kwenye ofisi za serikali za mitaa au ofisi za NEMC," amesema Waziri Jafo.
Hatua hiyo imekuja kutokana na kuongezeka kwa malalamiko ya kelele na mitetemo mwaka 2021/2022 ambapo asilimia 65 ya malalamiko yaliyowasilishwa NEMC yanahusu kelele na mitetemo, hali inayoonesha adhabu za kutozwa faini kwa wanaokamatwa zimezoeleka na hazitoshi.






