Ijumaa , 19th Sep , 2025

Helikopta iliyokuwa imembeba Rais wa Marekani Donald Trump ililazimika kuelekezwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Luton alipomaliza ziara yake ya kiserikali nchini Uingereza.

Waziri wa Vyombo vya Habari wa Ikulu ya White House, Karoline Leavitt alisema kutokana na tatizo dogo, ndege hiyo ilitua kwenye uwanja wa ndege wa ndani kabla ya kufika Stansted karibu dakika 20 nyuma ya ratiba.

Alisema uamuzi huo ulichukuliwa "kutokana na tahadhari nyingi" na kuongeza kuwa rais na mke wake "walipanda salama helikopta nyingine.

Huduma za dharura zilionekana kwenye lami huko Luton kufuatia kutua kwa ndege hiyo.

Picha tofauti zinaonyesha helikopta zote mbili za Trump, nje kidogo ya barabara ya Luton.
Ndege iliyombeba rais inajulikana kwa jina la Marine One.

Helikopta hizo zimewekewa mifumo ya ulinzi wa makombora na kuziba rada pamoja na vifaa vya elektroniki vilivyoundwa kustahimili mapigo ya sumakuumeme ya mlipuko wa nyuklia.