Jumanne , 26th Aug , 2025

"Namfahamu vizuri (Kim) kuliko mtu yeyote, karibu, zaidi ya dada yake. Ninampenda sana, hatukuwa na tatizo."

Wakati wa mkutano na rais mteule wa Korea Kusini, Lee Jae Myung, Rais  wa Marekani Donald Trump amesema kuwa yuko tayari kukutana na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un kwa mara nyingine tena.

Trump, ambaye alikutana na Kim mara tatu wakati wa muhula wake wa kwanza, amesisitiza nguvu ya uhusiano wao wa zamani. "Sawa, nina uhusiano mzuri sana na Kim Jong Un. Tulikuwa na mikutano miwili ya kilele. Tulielewana vyema. Namfahamu vizuri kuliko mtu yeyote, karibu, zaidi ya dada yake. Ninampenda sana,  hatukuwa na tatizo." Trump alisema.

Rais Lee kwa upande wake ameelezea matumaini yake kuwa Trump anaweza kuwa ufunguo wa kumaliza mzozo wa miongo kadhaa kwenye Peninsula ya Korea, akimtaja kuwa "mtu pekee" anayeweza kusuluhisha mzozo huo.

Wakati Vita vya Korea vikimalizika kwa mapatano katika miaka ya 1950, mkataba rasmi wa amani haukuwahi kusainiwa, na kuiacha peninsula hiyo kitaalam ikiwa bado iko vitani.

Hata hivyo, tangu Trump aondoke madarakani baada ya muhula wa kwanza na kurejea tena, Kim ameimarisha uhusiano na Moscow, na kutuma wanajeshi wa Korea Kaskazini kusaidia vita vya Urusi nchini Ukraine.

Korea Kaskazini imekataa mazungumzo mapya juu ya kutokomeza silaha za nyuklia na inaharakisha mpango wake wa silaha. Mwishoni mwa juma, Kim alilaani mazoezi ya hivi majuzi ya kijeshi ya Marekani na Korea Kusini, na kuyataja kuwa mazoezi ya uvamizi, na binafsi alisimamia majaribio ya mifumo mipya ya ulinzi wa anga.