Ijumaa , 24th Oct , 2025

Rais wa Marekani Donald Trump atakutana na mwenzake wa China Xi Jinping nchini Korea Kusini tarehe 30 Oktoba kando ya mkutano wa kilele barani Asia, 

Mkutano kati ya Xi na Trump umekuwa ukiandaliwa kwa wiki kadhaa huku mvutano kati ya mataifa hayo mawili yenye uchumi mkubwa duniani ukiendelea kuongezeka.

Utakuwa mkutano wa kwanza wa ana kwa ana kwa viongozi wote wawili tangu Trump arejee madarakani.
Trump ametishia kuweka ushuru wa ziada wa 100% kwa bidhaa za China kuanzia Novemba ikiwa China haitaondoa vikwazo vyake kwenye mauzo yake ya nje ya kemikali adimu.

China inatawala uzalishaji wa kemikali adimu na nyenzo zingine muhimu, ambazo ni sehemu muhimu katika magari, simu na vitu vingine vingi.

Katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Alhamisi, msemaji wa wa Ikulu ya White House Karoline Leavitt alithibitisha mkutano kati ya viongozi wote wawili.

Mkutano huo wa pande mbili utafanyika kando ya Mkutano wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia Pacific (Apec), utakaofanyika kuanzia tarehe 31 Okt - 1 Nov mwaka huu huko Gyeongju, Korea Kusini.

Trump pia anatazamiwa kukutana na kiongozi wa Korea Kusini Lee Jae Myung wakati wa safari yake nchini Korea Kusini, na kushiriki katika chakula cha jioni na viongozi.

Pia atakutana na viongozi kutoka Malaysia, Korea Kusini na Japan - hasa na Waziri Mkuu wake mpya Sanae Takaichi, amesema msemaji wa Ikulu ya White House.

Trump na Xi wamezungumza takribani mara tatu mwaka huu, karibuni zaidi ni mwezi Septemba, walipojadili makubaliano juu ya shughuli za TikTok nchini Marekani.

Walikutana 2019, wakati wa muhula wa kwanza wa Trump kama rais.

Trump amesema kuwa kuzungumza moja kwa moja na Xi ndiyo njia mwafaka zaidi ya kutatua mivutano inayoendelea kati ya Marekani na China, kama vile ushuru, migogoro ya kibiashara, usafirishaji haramu wa fentanyl na masuala mengine.