Ijumaa , 20th Mei , 2016

Tume ya Maendeleo ya Ushirika inakusudia kuvifuta katika daftari la vyama vya Ushirika vyama ambavyo vimekiuka matakwa ya Sheria ya Vyama vya Ushirika Na.6 ya mwaka 2013.

Dk. Audax Rutabanzibwa, Kaimu Mrajis wa Vyama vya Ushirika

Kwa mujibu wa sheria, Mrajis wa Vyama vya Ushirika, kwa mamlaka aliyopewa chini ya vifungu Namba 11(3), 8(2) na 100 anatakiwa kuvifuta vyama ambavyo vimeshindwa kufanya kazi katika kutimiza masharti ya usajili wake.

Masharti yaliyokiukwa ni pamoja na kutokufanya Mikutano kwa mujibu wa Sheria, kutokufanya chaguzi za viongozi kwa mujibu wa Sheria, kuwa na Idadi pungufu yawanachama na kushindwa kufanya shughuli zake kwa zaidi ya miezi sita, kinyumena matakwa ya Sheria na masharti ya vyama hivyo.

Kutokana na sababu hizo, vyama vinavyokusudiwa kufutwa ni 1,862 na vitafutwa baada ya siku tisini (90) kuanzia tarehe 13 Mei, 2016 siku ambayo Tangazo la Kusudio la Kufuta vyama hivyo lilipochapishwa katika gazeti la Serikali.

Idadi ya vyama vinavyokusudiwa kufutwa katika kila mkoa ni kama ifuatavyo: Arusha vyama 83, Dar es Salaam 91, Dodoma 50, Geita 16, Iringa 74, Kagera 240, Katavi 19, Kigoma 38, Manyara 73, Mara 203, Morogoro 278, Mtwara 52, Njombe 18, Pwani 324, Rukwa 14, Ruvuma 14, Shinyanga 89, Simiyu 93, Singida 15, Tanga 77 na Lindi 1.

Orodha ya vyama vinavyokusudiwa kufutwa inapatikana katika Ofisi za Ushirika za Wilaya na Mikoa na katika tovuti la Tume ya Maendeleo ya Ushirika (www.ushirika.go.tz ) .

Mtu yeyote au Taasisi yenye pingamizi la msingi dhidi ya kufutwa kwa chama husika, anatakiwa awasilishe pingamizi hilo na sababu zake katika Ofisi ya Mrajisikupitia Ofisi za Warajis Wasaidizi wa Mikoa husika ndani ya siku tisini (90) kuanzia tarehe 13/05/2016, siku ambayo tangazo la kufutwa kwa vyama hivyo lilipotangazwa katika gazeti la Serikali.

Umma unataarifiwa kwamba zoezi la kufuta Vyama vya Ushirika ambavyo haviendeshwi kwa mujibu wa Sheria ni endelevu na kwa ajili hiyo viongozi na wanachama wa vyama vya Ushirika na Maafisa Ushirika wanaagizwa kuhakikisha kwamba Vyama vya Ushirika katika maeneo yao viendeshwe kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Vyama vya Ushirika ili kuepuka vyama vyao kufutwa.