Jumatatu , 8th Jun , 2020

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Tundu Lissu leo Juni 8 ametangaza nia ya kugombea Urais katika Uchaguzi Mkuu.

Tundu Lissu

Amesema hayo kupitia ukurasa wake wa Facebook alipokuwa akizungumza na wananchi, ambapo ametoa ahadi kadhaa endapo atachaguliwa nafasi hiyo.

''Napenda kuwataarifu kuwa nimetangaza rasmi nia yangu ya kugombea nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi ujao mwezi Oktoba na nimeshawasilisha kila kitu kwa katibu mkuu wa chama chetu'', amesema Lissu. 

''Endapo nitachaguliwa kwenye uchaguzi ujao, nitahakikisha serikali yangu inaandaa sera nzuri ya kiuchumi, udhibiti wa mfumo wa bei ya vitu kwa maslahi ya wananchi na mfumo mzuri wa ukusanyaji mapato usiokandamiza wenye kipato cha chini'', amesema.

"Endapo nitachaguliwa, nitarudisha mamlaka ya Bunge kama zamani, nitaondoa vifungo na mateka yaliyowekwa kwenye mahakama zetu na nitaheshimu uhuru wa Mahakama katika wajibu wao wa kutenda haki''.

Kuhusiana na uhalali wake wa kugonmbea nafasi hiyo, Lissu amesema, ''mimi nina sifa zote za kuwania nafasi yoyote katika nchi hii na wala sijapoteza sifa hizo kutokana na Spika Job Ndugai kunifutia ubunge. Sijawahi kutuhumiwa wala kuthibitika kuwa na makosa mbele ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma''.

Waliojitokeza kuwasilisha fomu za kugombea Urais katika chama hicho mpaka sasa ni yeye Tundu Lissu pamoja na Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa.

Mtazame hapa.