Jumatano , 29th Mar , 2023

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema hadi sasa bado deni la serikali ni himilivu na lipo chini ya viwango vya ukomo huku akisisitiza kuwa serikali itaendelea kukopa kwa akili ili kuleta maendeleo

Kauli hiyo ameitoa leo wakati akipokea ripoti ya CAG na TAKUKURU ambapo amesema ili nchi ipate maendeleo ni lazima ikope ambapo amesema serikali itaendelea kukopa mikopo nafuu na kwa akili

“Mwenendo wa deni la serikali tunakopa ndio, tunakopa kwa maendeleo lakini tunakopa kwa akili, kama mlivyoona bado tupo chini wa viwango vya ukomo katika maeneo yote, tusipokopa kwa kuogopa hatutafanya maendeleo, lazima tukope mikopo yenye unafuu, na tuko vizuri”

Katika Ripoti ya CAG iliyokabidhiwa kwa Rais Samia leo imeeleza kuwa deni la serikali limeongezeka kwa trilioni 6.79
“Deni la serikali kufikia Juni 30/2022 ilikuwa ni shilingi trilioni 71.31 ikilinganishwa na shilingi trilioni 64.52 iliyoripotiwa kwa mwaka wa fedha 2020/2021 kuna ongezeko la shilingi trilioni 6.79”  amesema Charles Kichere, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali