
Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe.
Dkt.Mwakyembe ameingilia mgogoro huo ambao umedumu kwa takribani miaka saba sasa kuisababishia serikali hasara kubwa ya kimapato baada ya kutembelea ofisi za BAKITA na kukutana na tatizo hilo na kusema kuwa serikali haitakubali kuendelea kupoteza fedha zake kwa uzembe wa watu wachache.
"Sina mamlaka ya kuingilia Mahakama kwa kuwa kesi ipo Mahakamani lakini kinachonishangaza ni uongozi wa BAKITA kukaa kimya na kutouwajibisha uongozi wa BIMA ambao umechukua pesa takribani Bilioni 1.5 huu mwaka wa saba sasa. Warejeshe hiyo pesa nitahakikisha hiyo pesa inarudishwa lasivyo tutafikishana mbele kabisa mpaka katika viongozi wetu wa nchi kama hawatafanya maamuzi", alisema Mwakyembe.
Pamoja na hayo, Waziri Mwakyembe amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa BIMA pamoja na Katibu Mkuu wakutane kesho ili waweze kupata suluhu ya suala hilo na endapo hawatokea atachukua hatua dhidi yao.
"Wamepata maagizo yangu, kesho tuonane na endapo wasipotokea nitawaita sehemu ambayo wao wenyewe watakuja kwa mbio tena kwa miguu, hatuwezi kufanya mzaha mzaha, hii nchi sasa hivi inafuta upuuzi wote tuliyouzoea, hatuwezi kujenga nchi ya viwanda kwa mzaha wa aina hii", alisisitiza Dkt. Mwakyembe.
Kwa upande wake katibu mtendaji wa BAKITA Dkt.Seleman Sewangi amesema wameomba msaada wa serikali katika utatuzi wa tatizo hilo ili kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa uhuru.