Alhamisi , 20th Nov , 2014

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohamedi Gharib Bilal amesema nchi nyingi za Afrika ikiwemo Tanzania zimeshindwa kukuza uchumi wake kutokana na kutohimiza ujenzi wa viwanda

Dkt Abdallah Kigoda, Waziri wa Viwanda na Biashara

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohamedi Gharib Bilal amesema nchi nyingi za Afrika ikiwemo Tanzania zimeshindwa kukuza uchumi wake kutokana na kutohimiza ujenzi wa viwanda ambavyo ndio chachu ya kuleta mageuzi ya kiuchumi.

Makamu wa Rais amesema hayo leo jijini Dar es salaam katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Abdallah Kigoda katika maadhimisho ya siku ya viwanda barani Afrika.

Amesema nchi za Afrika kama zinataka kuleta mageuzi ya uchumi na kuleta maendeleo katika nchi hizo ni wajibu wao sasa kuhakikisha wanahimiza ujenzi wa viwanda ambapo pamoja na mambo mengine pia vitasaidia kutengeneza ajira kwa vijana katika nchi husika.

Wakati huo huo Shirika la kuhudumia viwanda vidogo nchini Tanzania (SIDO) limesema wazalishaji wadogo hapa nchini wanakabiliwa na matatizo makubwa ikiwemo lile la maeneo ya kuzalisha bidhaa zao kutokana na wengi wao kutokuwa na maeneo rasmi.

Meneja Masoko wa SIDO Bw. Henrick Mdede amesema tatizo hilo pia limekuwa likichangiwa na mitaji midogo waliyokuwa nayo wazalishaji hao wadogo na hivyo kupelekea kuchukua maamuzi ya kujenga viwanda vyao hata katika maeneo yasiyo rasmi.

Kutokana na changamoto hiyo Bw. Mdede ameziomba taasisi za fedha hapa nchini kusaidia wazalishaji hao wadogo wa bidhaa za viwandani kwa kuwapa mikopo yenye riba nafuu.

Tags: