Ijumaa , 14th Oct , 2022

Benki ya Dunia imeimwagia sifa Tanzania kwa usimamizi mzuri wa uchumi na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayopata fedha kutoka kwenye taasisi hiyo ikilinganishwa na nchi nyingine nyingi za Afrika.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt Mwigulu Nchemba, akia na ujumbe kutoka Tanzania

Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayesimamia Kundi la Kwanza la nchi za Kanda ya Afrika Dkt. Taufila Nyamadzabo, alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Tanzania, unaoongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.

Dkt. Nyamadzabo amesema kuwa Tanzania ni nchi ya mfano katika usimamizi wa uchumi ambapo licha ya majanga ikiwemo changamoto za UVIKO-19 na vita inayoendelea baina ya Urusi na Ukraine, tathimini inaonesha kuwa uchumi wa Tanzania uko imara na nchi inakopesheka.

Aliahidi kuwa Benki yake itaendelea kuisaidia Tanzania katika jitihada zake za kukuza uchumi na kuwaondolea umaskini wananchi wake kwa kusaidia rasilimali fedha zitakazotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, alimweleza Mkurugenzi huyo Mtendaji wa Benki ya Dunia anayesimamia Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika, Dkt. Taufila Nyamadzabo kwamba uchumi wa Tanzania unazidi kuimarika na kwamba Serikali itaendelea kuchukua hatua muhimu kuhakikisha uchumi unazidi kuimarika na kuleta ahueni kwa wananchi.

Alifafanua kuwa katika robo ya kwanza ya mwaka 2022/2023 uchumi umekua kwa asilimia 5.4 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 5.0 katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha uliotangulia 2021/2022 na kwamba kutokana na mipango kabambe iliyowekwa na serikali uchumi utakua zaidi hadi kufikia wastani wa asiliia 6.3.