Ijumaa , 3rd Aug , 2018

Idara ya Uhamiaji inadaiwa kuishikilia hati ya kusafiria (passport) ya  Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Twaweza, Aidan Eyakuze ambaye aliiwasilisha mwenyewe baada ya kutakiwa kufanya hivyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Twaweza, Aidan Eyakuze.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi huyo wakati akizungumza na wanahabari leo Agosti 3, 2018 na kudai kuwa suala hilo halitawayumbisha, na wataendeleza majukumu yao kama kawaida.

"Niliombwa nifike Uhamiaji na kupeleka pasi ya kusafiria, nikatekeleza, lakini mpaka leo sijapata maelezo wala barua ya kwanini washikilie pasi yangu, niliomba pasi ya muda niende Nairobi kikazi lakini nilinyimwa", amesema Eyakuze.

 Sanjari na hayo Eyakuze amebainisha kuwa Twaweza hawajapata taarifa ya kuwepo kwa kesi mahakamani, na barua waliyoandikiwa na COSTECH hawakutaja ule utafiti, wao walihoji juu ya uhalali wa utafiti wa sauti za wananchi, na waliichukua kama sehemu ya kazi zao na kudai kuwa wataendelea na kazi zao kama awali.

www.eatv.tv imemtafuta Msemaji wa Idara ya Uhamiaji, Ally Mtanda ili kufahamu sababu za kushililiwa kwa hati ya kusafiria ya Eyakuze, bila mafanikio.

Julai 11, Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) iliiandikia barua Twaweza na kuitaka kutoa maelezo kuhusu kibali cha kufanya utafiti, baada ya kuripoti utafiti ambao ulionyesha kuporomoka kwa ukaribu wa wananchi na vyama vya siasa, utekelezaji wa majukumu kwa viongozi walioko madarakani, Rais anavyotekeleza majukumu yake tangu alipoingia madarakani na uhuru wa kujieleza katika baadhi ya maeneo.