Alhamisi , 21st Mei , 2015

Serikali imesema kuwa uharibifu wa ardhi ni tishio kubwa kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi na unasababisha kupungua kwa uzalishaji wa chakula, kuzorota kwa mazingira na kupotea kwa viumbe hai.

Waziri wa Nchi , Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Dkt Binilith akizunguza na waandishi wa habari.

Kauli hiyo imetolewa jana na Waziri wa nchi ofisi ya makamu wa Rais (Mazingira) Dk, Binilith Mahenge wakati wa uzinduzi wa taarifa ya program ya taifa ya kukabiliana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame, mwongozo wa kuhuisha program ya taifa ya kupambana na kuenea kwa hali ya jangwa katika sera, mipango na program ya kisekta, taarifa ya hali ya uharibifu wa ardhi nchini na kitabu cha mbinu bora ya usimamizi endelevu wa ardhi mjini hapa.

Dk, Mahenge amesema kuwa robo ya uso wa dunia inatishiwa na kuenea kwa hali ya jangwa na eneo la zaidi ya hekta 3.2 bilion tayari limeathirika hali inayosababisha changamoto kubwa za kiuchumi, kijamii na kimazingira kwa zaidi ya watu million 900 duniani kote ambapo barani Afrika pekee tishio la jangwa ni wastani wa aslimia 73.

Amesema Jitihada za kukabiliana na uharibifu wa ardhi kwa kiasi zinakwamishwa na ukosefu wa takwimu za kutosha na za kuaminika kuhusu kiwango na ukubwa wa tatizo

Amengeza kuwa, Katika ngazi ya kitaifa inakadiriwa kuwa karibu asilimia 75 ya nchi ni kame, ambapo katika baadhi ya maeneo uharibifu wa ardhi ni wa kiasi kikubwa na unaendelea kupunguza tija ya ardhi

Ameyataja maeneo yaliyoathirika kuwa ni pamoja na mikoa ya Dodoma, Shinyanga, Simiyu, Singida, Mwanza, Mara, Tabora, Kilimanjaro, Manyara na Arusha.

Kwa upande wake Katibu wa Makamu wa Rais Mazingira, Sazi Salula alisema kuwa jumla ya dola za Marekani billion 10.2 zinakadiriwa kupotea kila mwaka kutokana na uharibifu wa ardhi nchini.

Hata hivyo amesema kuwa serikali imeshachukua hatua mbalimbali za kupambana na uharibifu wa ardhi zikihusisha uandaaji na utekelezaji wa sera, mikakati na mipango mbalimbali ya Kitaifa kukuza mbinu endelevu za usimamizi wa ardhi na uboreshaji wa mifumo ya usimamizi wa mifugo.

Pamoja na jitihada hizo tatizo la uharibifu wa ardhi na madhara yake bado yameendelea kuwepo hali hii inatoa wito wa juhudi zaidi za pamoja ili kupunguza ukubwa wa tatizo.