Ijumaa , 2nd Jan , 2026

Awali Ujerumani ilikuwa imeombwa, lakini ikaomba Ufaransa ihusishwe, jambo ambalo Libya ililikataa.

Libya imethibitisha kuwa Uingereza itakichambua kifaa cha kurekodi taarifa za safari (black box) kutoka kwenye ajali ya ndege iliyotokea Uturuki mwezi uliopita, ambayo iliua ujumbe wa juu wa kijeshi wa Libya, akiwemo mkuu wa jeshi Jenerali Mohammed al-Haddad.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Tripoli, Waziri wa Uchukuzi Mohamed al-Chahoubi amesema kuwa Libya na Uturuki zimeikubalia Uingereza kufanya uchambuzi huo, kwa kuzingatia sheria za kimataifa za usafiri wa anga.

Ameongeza kuwa awali Ujerumani ilikuwa imeombwa, lakini ikaomba Ufaransa ihusishwe, jambo ambalo Libya ililikataa.

“Kwa mujibu wa Mkataba wa Chicago, nchi inayochambua black box ni lazima isiwe imeengemea kwenye mrengo wowote, Ufaransa ni nchi iliyotengeneza ndege hiyo, na wahudumu wa ndege walikuwa pia Wafaransa, hivyo Ufaransa haina sifa ya kushiriki”, amesema al-Chahoubi.

Jenerali Haddad na wasaidizi wake wanne walifariki tarehe 23 Desemba wakati ndege yao aina ya Falcon 50 ilipoanguka muda mfupi baada ya kuruka kutoka Ankara, huku maafisa wa Uturuki wakitaja hitilafu ya mfumo wa umeme kuwa chanzo cha ajali. Wafanyakazi watatu wa ndege, wakiwemo raia wawili wa Ufaransa, pia walipoteza maisha. Kifaa cha kurekodi safari kilipatikana baadaye karibu na eneo la ajali.

Mamlaka za Libya zinasema Uingereza imekubali rasmi kutoa msaada wa kiufundi na kisheria katika uchunguzi huo, na matokeo yatatangazwa hadharani baada ya uchambuzi kukamilika.