Ukweli kufungwa makampuni ya Mo Dewji

Alhamisi , 18th Oct , 2018

Uongozi wa makampuni ya 'MeTL' unaomilikiwa na mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Dewji umekanusha taarifa za uvumi juu ya kusitisha shughuli za uzalishaji kwenye makampuni kufuatia tukio la kupotea kwa mmiliki wake Alhamis ya wiki iliyopita.

Mfanyabiashara Mohamed Dewji.

Taarifa za kusitishwa kwa uzalishaji wa makampuni hayo zilianza kusambaa hivi karibuni kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii, zikiinukuu makampuni juu ya azma yake ya kusitisha uzalishaji ifikapo Octoba 20 mwaka huu.

Kupitia mitandao yake ya kijamii, MeTL imeandika, “tunaendelea kusikitishwa na tukio lililomtokea Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni yetu, Mohammed Dewji. Pia tunapenda kutoa taarifa kwamba taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kuwa tarehe 20/10/2018 tutasimamisha shughuli za uzalishaji katika makampuni yetu siyo za kweli.”

Afisa Mtendaji Mkuu wa makampuni hayo, Mohamed Dewji alitekwa na watu wasiojulikana Alhamisi ya wiki iliyopitana mpaka sasa hakuna taarifa rasmi za kupatikana kwake licha ya Jeshi la Polisi kuwashikilia na kuwahoji watu 26.

Mapema wiki hii, familia ya mfanyabiashara huyo ilitangaza kutoa kitita cha shilingi bilioni 1 kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa za kupatikana kwa mfanyabiashaa huyo, ambaye inatajwa kupitia makampuni yake ameajiri zaidi ya wafanyakazi elfu 25 nchi nzima, akichagia asilimia 3.5 ya pato la taifa.