
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega
Amesema serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, imejipanga kutumia fursa za uchumi wa buluu zilizopo ndani ya Ziwa Victoria kuwawezesha vijana kufuga samaki kwa kutumia vizimba na kuuza samaki hao ndani na nje ya nchi ili kujiongezea kipato.
"Rais Samia ametoa bilioni 20 kwa ajili ya kuwezesha vijana kufuga samaki katika vizimba, hivyo ni wakati sasa wa kujipanga ili pesa hizo zitakapokuja tuweze kuzitumia vizuri kufanya uzalishaji wa samaki kwa wingi ili tuweze kuuza na kupata kipato", amesema Waziri Ulega
Ameongeza kuwa samaki aina ya Sato wanahitajika sana ndani na nje ya nchi, uhitaji ni mkubwa hivyo vijana wajipange vizuri ili waweze kutumia fursa hiyo kujiinua kimaisha.
Kwa upande wa vijana wanaojishughulisha na ufugaji wa samaki, Bahati Paul kutoka Ilemela na Peter Emmanuel kutoka Ukerewe kwa nyakati tofauti wamesema kuwa mpango huo wa serikali wa kuwawezesha vijana utasaidia sana vijana kujiajiri na kuondokana na changamoto ya ukosefu wa ajira.