
Waziri, Ummy Mwalimu
Ameyasema hayo wakati wa kilele cha wiki ya usafi wa mazingira ulioenda sambamba na mkutano uliojumuisha Maafisa Afya nchini na Wadau mbalimbali wa maendeleo kilichofanyika jijini Dodoma.
Wakati akitaja washindi waliofanya vizuri katika Halmashauri za Miji, Majiji, Wilaya, Vitongoji na Vijiji viliyofanya vizuri katika mashindano ya afya na usafi wa mazingira ambayo Wizara imekuwa ikitekeleza tangu mwaka 1988, Ummy Mwalimu amesema, “Mashindano hayo huanza katika ngazi ya Kitongoji na kuhitimishwa kwa kupata washindi wa kitaifa. Kila mwaka tumekuwa tukiboresha mashindano haya ambapo kwa mwaka huu tumeongeza makundi manne kutoka sita ya awali".
"Makundi yalioongezeka ni; Hospitali za Rufaa za Binafsi, Shule za Msingi za Vijijini, Shule za Sekondari za Bweni za Serikali, na Shule za Sekondari za Bweni za Binafsi”, ameongeza Waziri Ummy.
Aidha, waziri huyo alitaja makundi ya washindi waliofanya vizuri na makundi ya Halmashauri, Majiji na Mikoa iliyofanya vibaya.
Katika kundi la Halmashauri za Manispaa na Majiji lilihusisha Manispaa 25, ambapo Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ilikua kinara kwa asilimia 92.7, ikifuatiwa na mshindi wa pili Halmashauri ya Jiji la Arusha asilimia 90.5 na mshindi wa tatu ikiwa ni Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa asilimia 89.7. Kundi la pili lilikua la Halmashauri za Miji ambapo lilihusisha Halmashauri za miji 22 nchini, ambapo Mshindi wa kwanza ni Halmasahuri ya mji wa Njombe asilimia 93.4, Halmashauri ya Mji wa Kahama ikishika nafasi ya pili kwa asilimia 75.0 na Halmashauri ya Mji wa Tunduma ikiwa nafasi ya tatu kwa asilimia 73.5.
Kundi la tatu la Halmashauri za Wilaya, ambapo mshindi wa kwanza ni Halmasahuri ya Njombe ikiongoza kwa kupata asilimia 98.3, Kundi la nne lilihusisha Halmashauri za Vijiji ambapo vilishiriki vijiji 47 kwa wastani wa vijiji viwili kwa kila Halmashauri ya Wilaya iliyoshiriki. Kiongozi wa kundi hili ni Kijiji cha Ikuna, Kata ya Ikuna, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe asilimia 97.3.
Waziri Ummy alitaja mgawanyo wa zawadi zilizotolewa ni pamoja na Tuzo Maalum, Trekta yenye Tela, Gari (FWD) Ford Ranger, Vyeti vya ushindi, pamoja na Pikipiki. Zawadi hizo zilitolewa kulingana na makundi kumi yaliyoshindanishwa kuanzia ngazi za Vijiji hadi Halmashauri za Majiji na Manispaa.