Jumamosi , 20th Jul , 2019

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Julai 20, amezindua safari za Treni ya mizigo kutoka Tanga hadi Kilimanjaro, safari ambayo ilikuwa imesimama kwa takribani miaka 12.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Akizungumza katika hotuba yake mjini Moshi, Waziri Mkuu ameitaka elimu zaidi itolewe kwa wananchi, ili kuepusha ajali zisizo na Msingi, huku akisisitiza Sheria ya reli itolewa ipasavyo, ili wananchi waweze kuielewa kwa ufasaha.

''Tunasheria ambayo wananchi wengi hawaijui, kama Treni imekugonga sheria inasema, Treni haijakugonga ila wewe ndiyo umeigonga,  kwahiyo mjiepushe maana itakuwa inawaumiza sana, usidhani ukigongwa utalipwa fidia.'' amesema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Aidha waziri Mkuu ameagiza, vibarua walioshiriki vyema na kwa weledi, katika ujenzi wa reli hiyo wanapata ajira za moja kwamoja .

''Wale mtakaopata ajira, endeleeni kuwa mabalozi wazuri, Serikali imeridhia kabisa mpate ajira moja kwa moja kutokana na uaminifu, weledi na uchapakazi wenu katika kazi hii'' amesema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la reli nchini (TRC), amesema, mara ya mwisho Treni ya mizigo kuwepo ni miaka 12 iliyopita, na Treni ya mwisho ya abiria ilikuwa 1994,  ambapo Treni ya mwisho ya abiria kwenda Arusha ilikuwa 1983, na kwamba wamedhamiria kuzirejesha treni zote, ili kuweza kukuza uchumi wa watanzania.