Alhamisi , 23rd Feb , 2023

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, ametangaza vijana 812 kukubaliwa kati ya vijana 20,227 walioomba kushiriki mafunzo ya kujiunga na mradi wa kilimo wa vijana unaojulikana kama Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) huku mkoa wa Dar es Salaam ukiongoza kuwa na waombaji wengi.

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe

Wizara ya Kilimo ilitoa tangazo kwa umma kwa ajili ya vijana kuwsilisha maombi ili kujiunga na mafunzo ya kilimo biashara katika vituo atamizi ambapo dirisha lilifunguliwa Januari 10 mwaka huu na kufungwa Januari 30 mwaka huu huku jumla ya waombaji 20,227 wakijitokeza kati yao wanawake wakiwa 4,722 sawa na asilimia 23.34.

"Tayari Wizara imekamilisha taratibu za uchambuzi na kuwapata vijana hao watakaoshiriki mafunzo kwa awamu ya kwanza kati yao wanawake wakiwa 282 sawa na asilimia 34.73 na wanaume 530 sawa na asilimia 65.27," amesema Waziri Bashe

Aidha Waziri Bashe amesema vijana waliochaguliwa watapata mafunzo kwa kipindi cha miezi minne katika vituo 15 vilivyoandaliwa kuanzia machi 17 mwaka huu bila kukosa ambapo serikali itagharamia chakula, malazi na gharama za mafunzo.

Waziri Bashe amesema Rais Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kufungua mafunzo ya awamu ya kwanza Machi 20, mwaka huu jijini Dodoma.