Jumatano , 2nd Jul , 2014

Vijana Wilayani Mbarali Mbeya waitaka serikali kutangaza matumizi ya viroba na vipodozi vyenye viambata vya sumu kuwa ni janga la kitaifa.

Madawa na viroba yenye viambata vya sumu yakiteketezwa.

Vijana wilayani mbarali wameiomba serikali kutangaza tatizo la matumizi ya vipodozi vyenye viambata vya sumu na pombe haramu za viroba kuwa janga la kitaifa kama ilivyo kwa dawa za kulevya kutokana na matumizi ya bidhaa hizo kuwa na madhara makubwa kwenye sekta ya afya na uchumi wa taifa.

Wakizungumza wakati wa zoezi la kuteketeza vipodozi vyenye viambata vya sumu na pombe haramu za viroba ambalo limefanywa na mamlaka ya chakula na dawa TFDA wilayani mbarali, vijana hao wamesema matumizi ya vitu hivyo yamesababisha vijana wengi wilayani humo kupoteza maisha na wengine wengi kuadhirika hivyo kuitaka serikali itangaze kuwa matumizi ya Viroba na vipodozi hivyo ni janga la taifa.

Kaimu meneja wa mamlaka ya chakula na dawa kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Yusto Walace amesema TFDA itaendelea kudhibiti bidhaa hizo haramu huku baadhi ya maofisa wa serikali wilayani Mbarali wakielezea changamoto zinazowapata katika kukabiliana na bidhaa hizo.

Mkuu wa wilaya ya mbarali, Gulam Hussein Kifu amekiri kuwepo kwa bidhaa hizo kwa wingi wilayani Mbarali na kuitaka TFDA kutumia vyombo vya dola kuendeleza mapambano ya kuzidhibiti ili kupunguza madhara yake kwa vijana.