Jumapili , 5th Feb , 2023

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia  imeweka zuio la matumizi  ya vitabu visivyo na maadili ya kitanzania mshuleni ili kuendelea kusimamia utoaji wa elimu na kuhakikisha njia mbalimbali za ufundishaji zinazingatia ubora na maslahi ya nchi

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Francis Michael amesema kumekuwa na shule ambazo zinaingiza nchini vitabu ambavyo maudhui yake hayaendani na mila, desturi na utamaduni wa kitanzania.

Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya baadhi ya mitandao ya jamii kusambaza vitabu vinavyokinzana na mila na tamaduni za Tanzania, ikiwemo kuhamasisha mahusiano ya jinsia moja.

"Orodha ya vitabu hivyo itakuja kutolewa na Waziri wa Elimu kwa sababu yeye ndio mwenye Mamlaka hiyo kisheri ila niseme tu shule ambazo zitaendelea kukaidi na kuendelea kutumia vitabu ambavyo haviendani na mila,desturi na utamaduni vya nchi yetu  zitapata adhabu"amesema Dkt.Francis 

Pia Dkt.Francis amewakumbusha wamiliki wa shule hapa nchini kuzingatia sheria na taratibu na kuhakikisha wanatumia vitabu vya kiada na ziada ambavyo vinafuata miongozo ya kitanzania la sivyo adhabu kali zitatolewa ikiwemo kuzifungia na kuzifutia usajili shule husika