Jumapili , 27th Dec , 2020

Wamiliki wa vyuo binafsi vya kada ya famasi nchini wametakiwa wasibadilishe vyuo vikawa kama biashara kwani Serikali inatarajia kupata wataalam ambao wataweza kutoa huduma zinazostahili kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Msajili wa Baraza la Famasi Bi. Elizabeth Shekalaghe.

Wito huo umetolewa na Msajili wa Baraza la Famasi Bi. Elizabeth Shekalaghe ofisini kwake jijini Dodoma, ambapo amesema kuwa kila mwaka idadi ya vyuo inaongezeka na hadi sasa Baraza limeidhinisha vyuo 52 ngazi ya cheti hadi diploma ambavyo tayari vimesajiliwa na NACTE hivyo lazima kuwe na aina ya wataalam wenye uwezo ambao wanaendana na mahitaji ya sasa.

"Kama Baraza la Famasi tunao wajibu wa kusimamia kwa umakini  vyuo ili kuhakikisha  ubora wa mafunzo yatolewayo iendane na mitaala na mahitaji kulingana na hali ya sasa", amesema Bi. Shekalaghe

Kwa upande wa usimamizi wa maduka ya dawa muhimu,  Msajili huyo amesema baraza la famasi limekasimu baadhi ya majukumu katika ngazi ya halmashauri kwa mujibu wa sheria hivyo wameendelea kuendesha mafunzo kwa wakaguzi ili kuwakumbusha maadili,miiko na majukumu yao kama wafamasia na wakaguzi.

Bi. Shekalaghe,ameongeza kwa mwaka mpya ujao wamejipanga kumalizia kuwajengea uwezo wakaguzi hao nchi nzima na suala hili litakua endelevu. Amewakumbusha wananchi kutojinunulia dawa kiholela kwa kuwa inaweza kuwasababishia madhara kiafya na hivyo ni vema wakafanya vipimo ili kupata tiba sahihi.