Jumanne , 10th Dec , 2019

Wakala wa Vipimo Nchini (WMA), imesema kuwa itaendelea kulinda maslahi ya watumiaji na wafanyabiashara, kupata stahiki sahihi katika manunuzi na uuzaji wa bidhaa zao kwa kutumia vipimo vinavyoendana na thamani ya pesa inayolipwa na mteja.

Kaimu Meneja Wakala wa Vipimo Mkoa wa Temeke, Bw.Krishna Mahamba, akiwa kwenye Ukaguzi wa Nyama.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam katika ziara ya kushtukiza kwa wafanyabiashara wa mabucha, Kaimu Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Temeke, Krishna Mahamba, amesema kuwa dhumuni la ziara hiyo ni kuangalia kama vipimo vinazingatiwa na wauzaji ili kuleta usawa kwa wateja na wauzaji hao.

Katika kuadhimisha miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika, Wakala wa Vipimo tumeamua kufanya zoezi hili ambalo linafanyika Nchi nzima ili kulinda haki za biashara kwa wateja na wauzaji kwenye mabucha haya, kwani mara nyingi katika siku za sikukuu kama hizi wauzaji huwa wanachezea vipimo" amesema Krishna.

Ameeleza kuwa wafanyabiashara wa mabucha, wanapaswa kutumia mizani iliyopimwa ili kumuwezesha mteja kupata bidhaa inayolingana na thamani yake ya pesa.