Jumatano , 14th Dec , 2016

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof.Makame Mbarawa ameahidi kutoa shilingi milioni 100 kuwalipa mishahara wafanyakazi wa kampuni ya huduma za meli nchini Marine Mkoani mwanza kwa mwezi Desemba.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akiongea na wananchi jijini katika ziara yake Mwanza

Hatua hiyo ni baada ya kampuni hiyo kushindwa kulipa wafanyakazi wake mishahara ya miezi 11 iliyopita ambapo wafanyakazi wa kampuni hiyo kupitia kaimu mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo Eric Hamis kuwasilisha changamoto zinazoikabili kampuni hiyo kwa waziri likiwemo la swala la wafanyakazi kutolipwa mishahara yao.

Awali mkurugenzi huyo alisema kampuni inakabiliwa na changamoto nyingi hasa swala la mishahara ambapo takribani miezi kumi na moja wafanyakazi hao hawajapata hata shilingi moja kama sehemu ya mshahara wao hivyo kuwafanya wafanyakazi hao kuishi kwa shida.

Kutokana na kilio hicho waziri ametoa ahadi ya kutoa shilingi milioni 100 huku akiipa kampuni hiyo  jukumu la kutafuta shilingi milioni ishirini na nane ili kukamilisha jumla ya mshahara wanaopokea wafanyakazi hao ambapo jumla ya mshahara wa wafanyakazi wote kwa mwezi ni shilingi milioni 128, huku madai yao ya miezi 11 ya nyuma ikiwa ni jumla ya shilingi bilioni 1.2.