Jumatano , 11th Feb , 2015

Wafanyabiashara zaidi ya 600 wenye maduka makubwa na ya kati yaliyopo katika mitaa mbalimbali ya jiji hilo wameamua kufunga maduka yao na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wakazi wa jiji hilo.

Maelfu ya wakazi wa jiji la Mwanza kwa mara nyingine tena, wameendelea kuonja adha ya migomo, ambapo leo hii wafanyabiashara zaidi ya 600 wenye maduka makubwa na ya kati yaliyopo katika mitaa mbalimbali ya jiji hilo wameamua kufunga maduka yao na kuisababishia serikali hasara ya mamilioni ya shilingi.

Mgomo huo wa maduka ambao ulitangazwa kufanyika Februari 11 mwaka huu na viongozi wa jumuiya ya wafanyabiashara Mwanza ni hatua ya kumuunga mkono mwenyekiti wa jumuiya hiyo Tanzania Johnson Minja anayekabiliwa na kesi katika mahakama ya hakimu mkazi wilaya ya Dodoma.

Huduma za kibiashara katika jiji la Mwanza zilionekana kuzorota huku baadhi ya mitaa iliyozoeleka kwa pilikapilika za wananchi kufanya manunuzi ikiwa tulivu ambapo baadhi ya wafanyabiashara wamelalamikia hali hiyo.

Pamoja na kuwepo kwa mgomo huo, nimeshuhudia baadhi ya maduka kadhaa katika mtaa wa Uhuru na Liberty yakiendelea kutoa huduma, huku wengine wakilalamikia usumbufu uliojitokeza kutokana na kusafiri umbali mrefu kutoka katika visiwa vya wilaya ya Sengerema kuja Mwanza kutafuta mahitaji.