Jumanne , 5th Oct , 2021

Wafanyakazi wa Makampuni ya IPP Media leo wamepata nafasi ya kuchoma chanjo ya UVIKO-19, na kuwashauri watu wengine kuhamasika kuchoma chanjo kama walivyofanya wao kwa kuchoma chanjo hiyo kwa hiari, kama inavyoelekezwa na serikali.

Kushoto ni Afisa Uhusiano wa ITV Ayoub Semvua na kulia ni Mkurugenzi wa Makampuni ya IPP Abdiel Mengi

Wakizungumza mara baada ya kuchoma chanjo hiyo katika zoezi lililofanyika kwenye ofisi za EATV na ITV Mikocheni Jijini Dar es Salaam, baadhi ya wafanyakazi hao wamesema elimu kabla ya chanjo ni muhimu hivyo haina budi elimu kutolewa na wananchi kujitokeza kuchoma kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa wa Corona.

Kwa upande wake Mhudumu wa Afya kutoka kituo cha afya cha Magomeni, ambaye ndiye aliyeendesha zoezi la kuwachanja wafanyakazi waliojitokeza, ameitaja upotoshaji kwenye mitandao ya kijamii kuwa ndio kikwazo kikubwa kwa wananchi kuhamasika kwa urahisi kuchoma chanjo hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya Makampuni ya IPP Media, Mkurugenzi wa Makampuni hayo Abdiel Mengi, ameipongeza Wizara ya Afya kwa kurahisisha zoezi la utoaji wa chanjo na kuyaomba makampuni mengine yajitokeze kuhamasisha wafanyakazi wake kuchanja chanjo.