Jumamosi , 7th Dec , 2019

Rais Magufuli ameeleza kuwa alifanya juhudi za makusudi kwa kumtumia Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Patrick Mfugale, kukamilisha mchoro wa daraja la juu kwenye ziwa Victoria eneo la Kigongo Busisi lenye urefu KM 3.2.

Rais Magufuli

Akiongea katika hafla ya uwekaji wa jiwe la Msingi leo Desemba 7, 2019, Rais Magufuli amesema, mradi huo ni muhimu na anamshukuru Mfugale kwa kukamilisha mpango mapema pamoja na Bunge kwa kupitisha bajeti ya ujenzi huo.

'Nimeona nimtumie Mfugale haraka haraka, nikamwambia kamilisha mapema katika kipindi changu cha Urais inawezekana muda wangu ukiisha anaweza akaja Rais mwingine akaufuta huu mradi, na huyu Mfugale amekuwa akifanya vizuri katika miradi yote ya madaraja nchini', ameeleza.

Aidha Rais Magufuli amewaasa wananchi wa Mwanza hususani wa Wilaya za Sengerema na Misungwi ambapo mradi huo upo kuutumia vizuri kwa kunufaika kiuchumi kwani ni mradi muhimu kwa watanzania wote na nchi jirani.

Awali Mfugale alieleza kuwa mradi huo unagharimu Shilingi Bil. 699, ambazo zote ni fedha za ndani na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 40.