
Serikali imetoa vifaa vya TEHAMA katika Gereza Kuu la Uyui lililopo mkoani Tabora, kwa lengo kuwawezesha mahabusu na wafungwa kusikiliza mashauri yao kwa njia ya mtandao bila ya kulazimika kufika mahakamani.
Akikabidhi vifaa hivyo jana, Oktoba 20, 2025 Mkuu wa mkoa wa Tabora, Paul Chacha, amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa kupunguza muda na gharama za uendeshaji wa kesi.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Bi. Upendo Wella ameipongeza serikali kwa hatua hiyo, na kuongeza kuwa kutokana na shughuli nyingi kutegemea masuala ya kimtandao na teknolojia ya kisasa, bila vifaa wezeshi kazi inaweza isaifanyike kwa ufanisi, na kubainisha kuwa vifaa ambavyo vimetolewa vitakwenda kuhakikisha kazi inafanyika vyema
Naye, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Dkt. Adam Mambi amesema kuwa usikilizwaji wa mashauri kwa njia ya mtandao umerahisisha utoaji wa haki, na kwamba katika Kanda ya Tabora kwa mwaka 2024 hadi sasa, zaidi ya mashauri 421 yamesikilizwa kwa njia ya mtandao.
Mkuu wa Gereza la Uyui, ACP. Benard Balowa, amesema usikilizwaji wa mashauri mtandaoni Gerezani hapo utarahisisha utendaji pamoja na kupunguza usumbufu wa kwenda mahakamani kusikiliza kesi hizo.