Jumatano , 15th Mei , 2024

Kutokana na ukosefu wa huduma za afya katika kijiji cha Mwembeni, Kata ya Madanga Mkoani Tanga, wanawake wa kijiji hicho wamegoma kubeba ujauzito baada ya makubaliano na waume zao kwasababu wanapata shida wakati wa kujifungua kwani wanalazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma

Baadhi ya Wakazi wa Kata ya Madanga Mkoani Tanga

Kufuatia hatua hiyo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga Rajabu Abrahaman Abdallah amesema kuwa awali katika kijiji hicho palikuwa na zahanati ambayo ilijengwa chini ya kiwango cha ubora hali iliyopelekea serikali kuifunga kwa muda mfupi kutokana na majengo yake kuchakaa hivyo kuwalazimu wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma za Afya.

Bw. Abrahaman Abdallah amehimiza kuharakishwa kwa ujenzi wa Zahanati unaoendelea kijijini humo ili changamoto hiyo iweze kumalizwa na kuondoa matatizo ya wananchi yanayowakanbili kwa sasa. 

"Tayari shilingi milioni 28 zimetolewa na Zahanati imeshaanza kujengwa na ndani ya mwaka huu tutahakikisha inamalizika na kukamilika tayari kwa kuanza kutoa huduma, kwahiyo wakinamama wa Mwembeni ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, ruksa kubeba mimba sasa" alisisitiza Mwenyekiti Rajab. 

"Waliniambia wakinamama wa Mwembeni kwamba wamekubaliana na waume zao kwa muda sasa wasibebe ujauzito  kwasababu wanapata shida inapofika wakati wa  kujifungua kwakuwa wanakwenda mbali na muda lakini wakati mwingine wamekuwa  wanajifungulia njiani hali inayohatarisha afya zao, " alisema Mwenyekiti huyo.