Ijumaa , 5th Dec , 2014

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dk. Richard Sezibera, amewataka wahandisi wa nchi wanachama, kuhakikisha wanatumia taaluma yao kuboresha maisha ya wananchi wa EAC.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk. Richard Sezibera.

Wito huo aliutoa jana jijini arusha, wakati akifungua mkutano wa tisa wa kimataifa unaojadili jinsi ya kufikia malengo ya milenia 2015 na kukabiliana na changamoto zilizopo kabla katika nyanja ya uhandisi. amesema kuwa nchi zinazoendelea zikiwemo nchi hizo wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, zinakabiliwa na changamoto kubwa Nne, ambazo ni ukosefu wa umeme wa nishati ya jua, maji safi na salama,miundombinu ya miji na sekta ya afya ni shida kwa wananchi hasa wa vijijini.

Dk.Sezibera amesema kuwa hakuna maendeleo yoyote yatakafanyika bila kumuhusisha mhandisi, hivyo ni vyema wakaongeza juhudi katika kusaidia kukabiliana na changamoto hizo.

Naye makamu mwenyekiti wa taasisi ya wahandisi Tanzania, Mhandisi, Mussa Kimaka amesema sekta yao inakabiliwa na changamoto kubwa ya rasiliamali watu, fedha chache na muda uliopangwa wa kufikia malengo ya milenia ni mdogo hautoshi kutimiza malengo yote.

Amesema kuwa katika mkutano huo watajadili changamoto zote kubwa wanazokabiliana nazo na kuona jinsi watakavyoboresha ndani ya mwaka mmoja kabla ya kufikia muda wa malengo ya milenia 2015.