Jumatano , 25th Sep , 2019

Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Augustine Mahiga amesema maombi ya watuhumiwa ambao ni wahujumu uchumi yamekuwa yakiongezeka tangu Rais Magufuli atoe ushauri kuhusu kuachiwa kwa watuhumiwa wa makosa hayo wakiomba radhi.

Waziri Mahiga amesema washtakiwa wa makosa ya uhujumu uchumi wanapeleka maombi kwa kasi kwenda kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) wakiomba kutoka rumande.

"DPP Biswalo Mganga ameanza kupokea maombi kwa kasi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa pendekezo la Rais Magufuli, hapa nimetoka kuzungumza naye ameniambia maombi yanaingia kwa kasi sana na sasa lazima wafanye uchambuzi", amesema Waziri Mahiga.

"Mshtakiwa mwenyewe au kwa kupitia mawakili wake akiwa mahabusu ataandika barua ili kesho na kesho kutwa asije kuiruka serikali, ndiyo maana watuhumiwa wenyewe wanaandika", ameendelea kusema Waziri Mahiga.

Hivi karibuni wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua, Rais Magufuli alitoa siku 7 kwa DPP kupokea maombi ya watuhumiwa wa uhujumu uchumi wanaotaka kulipa faini.