Jumamosi , 22nd Nov , 2025

Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, ametoa tahadhari kwa mashabiki wa soka kuelekea mchezo wa kimataifa wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Simba SC na Petro Atletico ya Angola.

 

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa siku ya Jumapili, Novemba 23, 2025, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 10:00 jioni, na unatarajiwa kuvuta maelfu ya mashabiki kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

Akizungumza na vyombo vya habari, Kamanda Muliro amesema:  
“Jeshi la Polisi linatambua umuhimu wa mchezo huu na linawahimiza mashabiki wote kuzingatia sheria, kuepuka vitendo vya vurugu, fujo au uvunjifu wa amani. Tutaweka ulinzi madhubuti ili kuhakikisha usalama wa kila mmoja.”

Aidha, alisisitiza kuwa jeshi la polisi halitasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayekiuka taratibu za michezo au kujaribu kuvuruga amani.  

“Mashabiki wanapaswa kuonesha uzalendo na nidhamu kwa kuishangilia timu yao kwa amani. Tunawatakia mafanikio Simba SC katika mchezo huu muhimu.”

Jeshi la Polisi pia limewahimiza mashabiki kufika mapema uwanjani ili kuepusha misongamano na kuhakikisha ulinzi unakuwa wa uhakika kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mchezo.