Alhamisi , 18th Feb , 2016

Wakazi wa katika kijiji cha namba Nne wilayani Arumeru Magharibi wameiomba serikali kulitafutia ufumbuzi wa kudumu tatizo lao la ukosefu wa kituo cha afya, hivyo kuchangia wakina mama wajawazito kutohudhuria kliniki hali inayohatarisha maisha yao.

Diwani mpya wa kata Laroi,Ojungu Salekwa

Wakiongea kwa nyakati tofauti na East Africa radio baadhi ya wakazi hao wamesema kwa miaka mingi wamekuwa wakilazimika kutembea zaidi ya kilometa 30 kufuata huduma ya afya jambo ambalo limekuwa likigharimu maisha ya baadhi yao.

Wakizungumza kwa masikitiko makubwa baadhi wa wanawake wa eneo hilo wamesema licha ya jitihada kubwa zinazofanywa na serikali za kunusuru maisha ya mama mjamzito na mtoto, kata yao imekuwa ikishuhudia adha kubwa kwa wanawake na watoto kukosa huduma hizo muhimu.

Ojungu Salekwa ni diwani mpya wa kata Laroi, ambaye licha ya kukiri kuwepo kwa tatizo hilo pia, ameziomba taasisi na mashirika yasiokuwa ya kiserikali kujitokeza kuisaidia kata yake katika ujenzi wa kituo cha afya.

Licha ya jitihada zilizofanywa na wakazi wa kata hiyo za kuanza ujenzi wa kituo cha afya kwa miaka mingi ujenzi wa kituo cha afya umekwama katika ngazi ya msingi, ambapo hadi kukamilika kunahitajika zaidi ya shilingi milioni mia na hamsini.