Ijumaa , 21st Oct , 2022

Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde ameitaka Bodi ya Kahawa Tanzania kuweka mfumo madhubuti wa ufuatiliaji kwa wakulima wote wanaopewa miche bora ili iweze kuongeza tija na uzalishaji.

Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde

Naibu Waziri Mavunde ameyasema hayo wilayani Kyerwa alipokuwa akizindua zoezi la ugawaji wa miche bora 800,000 ya kahawa iliyozalishwa na kampuni ya JJAD na kugawiwa bure kwa wakulima kupitia serikali.

"Sisi kama Wizara, tumewapa Bodi ya Kahawa malengo ya kuzalisha miche milioni 20 kwa mwaka, lengo hilo tumeliweka ili kuendana na malengo ya ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025 ambayo imetuelekeza kufikia uzalishaji wa tani 300,000 za kahawa ifikapo 2025, hivyo, ni lazima Bodi ya Kahawa kufuatilia miche hii tunayogawa kwa wakulima ili iwe na tija na kuongeza uzalishaji," amesema Naibu Waziri Mavunde

Aidha Mavunde ameongeza kuwa, "Ndugu zangu wakulima, hakuna jambo la muhimu sana kwenu ambalo litarahisisha sana kwa serikali na wadau wote kutoa huduma kwenu kama tukiwatambua, hivyo, ninawaomba mtoe ushirikiano ili muweze kusajiliwa, mtambulike mpo wangapi ili muweze kupewa huduma stahiki kulingana na mahitaji yenu,"