Jumatano , 21st Mei , 2014

Siku moja baada ya watu wenye ulemavu kufunga makutano ya barabara za Uhuru na Kawawa kupinga kuondolewa katika maeneo waliyokuwa wanafanyia biashara zao, uongozi wa Mkoa wa Dar-es-Salaam umeanza kugawa maeneo kwa walemavu hao.

Baadhi ya walemavu ambao hapo jana walifunga makutano ya barabara za Uhuru na Kawawa kupinga kuondolewa kutoka katika maeneo waliyokuwa wakifanyia biashara.

Zaidi ya watu 200 watapata maeneo ya kufanya biashara pembeni mwa kituo cha mabasi cha Karume, katika zoezi ambalo litawanufaisha zaidi wafanyabiashara 200, wengi wao wakiwa walemavu wa viungo ambao hivi sasa watakuwa na eneo maalumu la kufanya shughuli za kuwaingizia kipato.

Akizungumza na East Africa Radio, mmoja wa viongozi wa watu wenye ulemavu ambaye alikuwa akihakiki majina ya wanaostahili kupatiwa maeneo hayo amesema wameridhishwa na hatua zilizochukuliwa na serikali na kuonya kuwa hawatakubali kuondolewa mpaka serikali itakapoandaa eneo rafiki kwa wao kufanyabiashara.