Jumatano , 17th Feb , 2016

Watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wakiwa wamevalia sare zinazofanana na jeshi la polisi wamewavimia na kuwajeruhi kwa kuwakatakata mapanga walimu watatu

Watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wakiwa wamevalia sare zinazofanana na jeshi la polisi wamewavimia na kuwajeruhi kwa kuwakatakata mapanga walimu watatu wa shule ya sekondari ya Mara iliyoko mjini Musoma mkoani Mara na kuwasababishia majeraha makubwa katika sehemu mbalimbali za miili yao.

Wakizungumza wakiwa wamelazwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mara mjini Musoma , walimu hao Vedastus Rwechungula, Juma Amos na Maccelo Ndege, wamesema tukio hilo limetokea majira ya saa nne hadi saa tano usiku wakati wakiwa njiani kurejea shuleni ikiwa ni mita chache tu kabla ya kufika shuleni hapo.

Wamesema kuwa vitendo vya uhalifu na uvamizi katika maeneo ya shule hiyo vimekuwa vikijitokeza mara kwa mara lakini licha na vyombo vya dola kupewa taarifa hizo hakuna hatua ambazo zimekua zikichukuliwa.

Kaimu mganga mfawidhi wa hospital ya rufaa ya mkoa wa Mara Elias Godfrey amethibitisha kuwapokea majeruhi hao watatu jana usiku, ambapo mmoja wapo hali yake si ya kuridhisha kutokana na panga alilokatwa sehemu ya kichwani kufika kwenye fuvu la kichwa.

Naye mkuu wa jeshi la polis wilaya ya Musoma, amekiri kupokea taarifa hizo za kukatwa walimu hao na kusema kuwa jeshi la polisi wilayani humo limejipanga kufanya msako mkali katika kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria watuhumiwa hao.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Musoma ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo Zerothe Stephen, ameliagiza jeshi la polisi kuhakikisha wahusika wote wa tukio hilo wanapatikana na kuchukuliwa hatua za kisheria…