Alhamisi , 11th Oct , 2018

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda amesema serikali ya Mkoa huo ipo katika mikakati ya kuingiza magari 20 maaulum kwa ajili ya wanafunzi wa mkoa huo ili kuwaondolea adha ya usafiri na kuwapa fursa ya kuwahi masomoni hususani nyakati za asubuhi.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda akizungumza na wananchi wa Kimara.

Makonda ameyasema hayo leo alipotembelea kituo cha mabasi yaendayo haraka kilichopo Kimara, Dar es salaam, ambapo ameahidi kulitatua suala la usafiri lililojitokeza kituoni hapo sambamba na kumaliza tatizo la usafiri kwa upande wa wanafunzi wa mkoa wa Dar es salaam kwa kuwapatia magari yao binafsi.

Kuna changamoto ya wanafunzi wanapata shida ya usafiri na wengi wao ni watoto, sisi kama serikali ya Mkoa tuna mpango wa kuingiza magari 20 maalumu kwaajili ya wanafunzi wetu ili watoto hao waweze kupata fursa ya kuwahi masomoni, na mpango huo endapo wakubwa zetu wakikubali tutaanza kutumia barabara za mwendokasi”, amesema Makonda.

Aidha Makonda amewaomba wananchi wanaotumia usafiri wa mwendokasi kuipatia serikali muda wa siku tatu kulitatua tatizo la usafiri huo, ambao umekuwa kero kwa wananchi wa maeneo ya jiji la Dar es salaam huku akiagiza kufungwa kamera katika vituo vyote vya mabasi nchini kwa lengo la kuzuia uhalifu.

Tunaomba watumiaji wa usafiri huu watupatie muda wa siku tatu ili sisi pamoja na uongozi wa mabasi haya tukishirikiana na kiongozi wetu Waziri wa TAMISEMI kulitatua tatizo hili kwani yeye ndiyo atakayetoa tamko mabasi yanaongezeka lini?, utaratibu wa nauli unafanyikaje?, na lini wananchi watalipa kwa kutumia kadi ili kuziba mianya ya wizi kwenye vituo vya mabasi”, ameongeza.

Pia Makonda ametoa ruhusa kwa abiria wanaotumia usafiri huo kupiga picha ndani ya vituo vya mwendokasi huku akitoa wito kwa wananchi kuripoti vitendo vyote vya unyanyasaji vinavyofanywa na askari pamoja na wafanyakazi vituoni hapo kwa kurekodi matukio hayo kwa kutumia simu zao ili waweze kuwachukulia hatua za kisheria.