Wananchi kumshtaki mwalimu aliyebaka mwanafunzi 

Jumatano , 25th Mar , 2020

Wananchi wa Kijiji cha Kasu, Kata ya Milundikwa wilayani Nkasi mkoani Rukwa wameiomba Serikali kumfikisha mahakamani mwalimu wa Shule ya Sekondari Milundikwa, Harry Katamba (37) kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi wake wa kidato cha pili mwenye umri wa miaka 17.

Shule ya Sekondari Milundikwa

Wakiongea na EATV na Radio Digital katika nyakati tofauti, wananchi hao wamelaani vikali kitendo hicho huku  wakisisitiza kuwa kuchukuliwa hatua kwa mwalimu huyo kutakuwa funzo kwa watu wengine wenye tabia chafu na ovu kama hiyo.

Mtendaji wa kijiji hicho, Benazilia Kalamba amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba mtuhumiwa amekamatwa na kufikishwa katika Kituo cha Polisi Namanyere kwa uchunguzi zaidi, kauli iliyoungwa mkono na Makamu Mkuu wa shule hiyo Charles Mwamengo.

Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa, Justin Masejo  amethibitisha kutokea  tukio  hilo, ambapo hivi sasa mtuhumumiwa amekamatwa na  upelelezi unaendelea.