Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Kighoma Malima, kufuatia vifo vya watu kumi katika ajali ya barabarani iliyotokea tarehe 31 Desemba, 2025 mkoani humo.
Ajali hiyo ilitokea katika Kijiji cha Maseyu, Kata ya Gwata, Wilaya ya Morogoro, kwenye barabara kuu ya Morogoro–Dar es Salaam ikihusisha basi la abiria lenye namba ya usajili T 1662 DMD aina ya Mitsubishi Fuso, mali ya Kampuni ya Bil Mawio, lililokuwa likisafiri kutoka Morogoro kwenda Tanga, na lori la mizigo aina ya HOWO lenye namba T 956 ELW, mali ya Kampuni ya Kikori. Magari hayo yaligongana uso kwa uso na kuteketea kwa moto.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, waliofariki dunia ni wanawake wawili na wanaume wanane, wote wakiwa abiria wa basi hilo, na majeruhi ni 23 waliopatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro. Kati yao, majeruhi 11 wametibiwa na kuruhusiwa, huku 12 wakiendelea na matibabu.
Miili tisa ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, na mmoja katika Kituo cha Afya Mikese. Kati ya hiyo, miili mitano imetambuliwa, huku mitano mingine ikiwa bado haijatambuliwa kutokana na kuharibika kwa majeraha ya moto. Wataalam wa uchunguzi wa vinasaba (DNA) wamechukua sampuli za miili hiyo kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Rais Dkt. Samia ametoa pole kwa familia za wafiwa na kuziombea roho za marehemu zipumzike kwa amani, pamoja na uponyaji wa haraka kwa majeruhi wote.
Aidha, amewataka madereva na watumiaji wa barabara kuzingatia kikamilifu sheria na kanuni za usalama barabarani.

