Ijumaa , 15th Feb , 2019

Changamoto ya upatikanaji wa huduma za Afya katika kijiji cha Nyang’holongo Kata ya Nundu Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale Mkoani Geita imekuwa kubwa, hali inayopelekea wananchi kukimbilia kwa waganga wa jadi kupata huduma hizo.

Baadhi ya vifaa vya waganga wa jadi

Imeelezwa kuwa sababu za baadhi ya wananchi kufuata huduma za matibabu kwa waganga wa jadi ni huduma za afya kuwa umbali mrefu kwani wanalazimika kutembea umbali wa kilomita 10 kwenda katika Zahanati ya kata jirani ya Bukwimba ama wanasafiri kwenda makao makuu ya Wilaya kwenye kituo cha afya Kharumwa takribani kilomita 25.

Marko Mwiyabule ni Mwenyekiti mwanzilishi wa kijiji hicho tangu mwaka 1974 na kustaafu mwaka 2004, ambapo  anasema wananchi wamekuwa wana mwamko hali iliyopelekea kuchangia  Sh. elfu sitini kwa lengo la kujenga zahanati ambapo afisa Mtendaji wa Nyang’holongo Masumbuko Robert amesema walifikisha milioni 22 ambazo walinyanyua boma.

Kutokana na changamoto hizo zinazowakabili wananchi, Mgodi wa Dhahabu wa Acacia Bulyanhulu kutoka Mkoani Shinyanga umeguswa na kutoa msaada wa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya zaidi ya Milioni 67.

Akipokea vifaa hivyo Mkuu wa wilaya ya Nyang’hwale, Hamimu Gwiyama amesema kiongozi kutoka ngazi ya wilaya kwa mara ya mwisho alifika kijijini hapo mwaka 2005 yapata miaka 14 sasa.

Aidha uongozi wa kijiji umesema kuna wakazi wapatao 2598 na kwamba waliochangia fedha kama nguvu za wananchi ni wakazi 502 hivyo wamejielekeza kuleta msukumo zaidi ya ili watu wote washiriki kikamilifu kwenye miradi ya maendeleo.