Jumatano , 16th Jul , 2014

Wakazi wa mtaa wa Ubungo Kisiwani jijini Dar es salaam nchini Tanzania wameilalamikia serikali ya mtaa huo kwa kushindwa kuchukua hatua za kudhibiti watu wanaotiririsha maji yenye kinyesi kwenye mfereji uliopita kati kati ya makazi ya watu.

Moja ya maji machafu yanayotiririka kuelekea makazi ya watu.

Wakizungumza na East Africa Radio wakazi wa mtaa huo wamesema licha ya viongozi kuona hali ya hatari ikiwemo ya uwezekano wa kupata magonjwa ya milipuko lakini wamekuwa hawachukui hatua za kudhibiti na hivyo kuwaacha wananchi wakiwa wanaishi katika hali ya wasiwasi.

Hata hivyo akizungumzia tatizo hilo diwani wa kata hiyo ya Ubungo Kisiwani Bw. Bonifasi Jakobo amesema tatizo la kuwepo kwa maji yeynye kinyesi ndani ya mfereji huo linatokana na baadhi ya watu wasiojulikana kufungulia maji hayo na kuyatiririsha katika mfereji huo.

Wakati huo huo, Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini Tanzania - TPDC, limesema mpaka sasa utafiti unaonesha kwamba kuna futi za ujazo bilioni 9.6 za gesi asilia.

Mkurugenzi wa TPDC Yona Kilagane amesema kati ya hizo, futi za ujazo bilioni 8 zipo kwenye nchi kavu huku futi za ujazo bilioni 42.2 zipo kwenye kina cha bahari kuu.

Kilagane amesema hayo leo jijini Dar es salaam wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwa lengo la kutolea ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu uchimbaji wa gesi asilia na utafiti kuhusu mafuta.