Ijumaa , 17th Jan , 2020

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera linawashikilia watu saba ambao ni Sophia Joseph, Joseph Magambo, Alphonce Karoli, Martine Makabe, Alex Leopord, Salvatory Mwiliza na Aloyce Leopord kwa tuhuma za mauaji ya wanandoa wawili huku chanzo kikielezwa kuwa ni mgogoro wa ardhi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Revocatus Malimi.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Revocatus Malimi, amesema kuwa tukio hilo lilitokea Januari 14, 2020, majira ya saa 7:00 usiku, katika Kijiji cha Mabale, Kata ya Nyakahura wilayani Biharamulo, ambapo wanandoa hao walikuwa wamelala na ndipo walipovamiwa na kundi kubwa la watu na kuanza kuwacharanga mapanga sehemu zao mbalimbali za miili yao.

"Kabla ya tukio hilo, kulikuwa na mgogoro wa ardhi kati ya marehemu na baadhi ya wana ukoo kwa muda mrefu, uliotokana na kuachiwa eneo alilokuwa akiishi na Babu yake, aliyehama kwa shinikizo la wana jamii waliomtuhumu kuwa ni mwizi" amesema Kamanda Malimi.

Wanandoa hao waliopoteza maisha yao ni Elizeus Rubanie (35) na mke wake, Juliana Joseph (28), na kwamba upelelezi utakapokamilika watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani.