Wanane waokolewa baada ya kufukiwa na kifusi

Jumanne , 10th Sep , 2019

Takribani watu wanane kati ya 10 ambao ni wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika mgodi wa Shilalo ulioko katika Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, wameokolewa wakiwa hai, baada ya kufukiwa na kifusi.

Picha haihusiani na tukio halisi lililotokea

Akizungumza na EATV&EA Radio Digital leo Septremba 10 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Jumanne Muliro, amesema kuwa, tukio hilo limetokea majira ya saa 7:00 usiku mara baada ya shimo namba 47 waliloingia kuelemewa na udongo na kisha kuporomoka.

''Baada ya tukio hilo kutokea, jitihada mbalimbali zilifanyika na kufanikiwa kuwaokoa watu wanane wakiwa hai, wawili wakawa bado ila baadaye mmoja aliokolewa akiwa amefariki tayari na juhudi hadi sasa zinaendelea ili kumuokoa huyo mmoja aliyebakia''. amesema Kamanda Muliro.

Kamanda Muliro ameongeza kuwa manusra wa ajali hiyo wamepelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Misungwi kwa ajili ya uchunguzi zaidi na kutoa wito kwa wachimbaji wadogo wadogo kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa uangalifu zaidi.