Jumatatu , 21st Jul , 2014

Jopo la mawakili, wanasheria na wanaharakati wa haki za binadamu, linakutana jijini Dar es Salaam kujadili maamuzi ya mahakama kuu, ya kutaka kituo cha Sheria na Haki za Binadamu - LHRC kiilipe sh bilioni 2.8 kwa kampuni ya kufua umeme ya Dowans.

Mkurugenzi mkuu wa LHRC Dkt Hellen Kijo-Bisimba.

Jopo hilo linaloongozwa na walakamikaji ambao ni kituo cha sheria na haki za binadam, linapitia na kuangalia mazingira ya kisheria, hasa namna mahakama kuu ya Tanzania ilivyokubali kuisajili tozo hiyo, kwa lengo la kukata rufaa katika mahakama ya juu kama anavyoeleza Mkurugenzi Mkuu wa LHRC Dkt Hellen Kijo-Bisimba.

Wiki iliyopita katika mahojiano maalumu na EATV, Dkt Bisimba amefafanua kuwa hatua yoyote ya kuisajili tozo hiyo ni sawa na kukifuta kabisa kituo hicho na kwamba watakaoathirika ni wananchi maskini wanaokadiriwa kufikia elfu Kumi na Tano ambao kituo hicho kimefungua kesi kwa niaba yao na zinazoendelea katika mahakama mbalimbali nchini.

Kwa mujibu wa Dkt Bisimba, kiasi hicho cha pesa ambacho LHRC inatakiwa ikilipe hakina uhalali wa kisheria kwani shauri walilofungua wao na asasi nyingine mbili pamoja na mwananchi wa kawaida mmoja, lililenga kuiepusha serikali isiingine gharama na kwamba aina hiyo ya mashauri haipaswi kutozwa gharama kutokana na kuwa na maslahi ya moja kwa moja kwa wananchi.

Chanzo cha gharama zinazodaiwa na Dowans ni kuhusu kesi iliyofunguliwa na LHRC pamoja na wenzake ya kupinga mahakama kuu isisajili tozo ya shilingi bilioni 98 ambazo shirika la umeme nchini Tanesco lilitakiwa liilipe kampuni ya Dowans kwa kosa la kuvunja mkataba pasipo kufuata sheria.
…............................................