Ijumaa , 28th Aug , 2015

Wanawake wachimbaji wa madini kutoka mikoa ya Tanga,Singida, Manyara na Morogoro wameiomba serikali ipunguze ada ya leseni ya uchimbaji madini ili kuwawezesha kinamama wanaoanza kazi hiyo wasikwame kiuchumi.

Pili Hussein ni mwanamama wa kwanza kuzama katika migodi ya Mirerani na kuchimba madini ambaye kwa sasa ni mmiliki wa kitalu cha madini.

Kinamama hao ambao wameamua kujikita kwenye shughuli za uchimbaji wa madini wameiomba serikali isikie kilio chao cha muda mrefu licha ya sekta hiyo kuwa bado inawasaidia kinamama kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umasikini.

Pili Hussein ni mwanamama wa kwanza kuzama katika migodi ya Mirerani na kuchimba madini ambaye kwa sasa ni mmiliki wa kitalu cha madini amesema kuwa gharama kubwa za uendeshaji wa migodi zimekuwa zikirudisha nyuma juhudi za kinamama hivyo ameiomba serikali na mashirika binafsi kujitokeza kuwasaidia kinamama kupata mikopo itakayowasaidia kuendesha shughuli za uchimbaji.

Wakizungumza katika jukwaa la kinamama wachimbaji wa madini linaloendelea mkoani Kilimanjaro lilioandaliwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la Hakimadini , jukwaa lenye lengo la kuunganisha sauti na nguvu ya kinamama katika kutetea haki zao hususan katika sekta ya madini na kunufaika ipasavyo.

Mwansy Shomari ni mchimbaji wa madini aina ya Ruby kutoka eneo la Kalalani mkoani Tanga amesema kuwa licha ya changamoto wanazozipitia mfumo dume umekuwa ukiwakwamisha kinamama kupiga hatua kiuchumi hususani katika sekta ya madini iliyotawaliwa na mfumo dume kwa kipindi kirefu.

Kwa upande wake Meneja Programu wa Shirika la Hakimadini, David Ntiruka amesema kuwa wameanzisha program maalumu ya kukusanya sauti ya kinamama wachimbaji pamoja na changamoto zao ili kuzifikisha kwenye vyombo husika viweze kufanyiwa kazi.

Mwamko wa wanawake kujihusisha na shughuli za uchimbaji madini bado unakuwa na kuongezeka ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo wanawake wachache walithubutu kujihusisha na uchimbaji ,kutokana na kuongezeka kwa uelewa juu ya haki ya kunufaika na madini kwa jinsia zote wanawake wengi wanashiriki katika uchimbaji madini.