Alhamisi , 12th Mei , 2016

Wananchi waishio katika wilaya ya Longido mkoani Arusha pamoja na wadau wa maendeleo wametakiwa kuinusuru na ukame kwa kupiga marufuku uchomaji mkaa na ukataji miti kwa kuhimiza utunzaji wa mazingira katika wilaya hiyo inayokabiliwa na uhaba wa maji.

Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari Mkoa wa Arusha Cloud Gwandu.

Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari Mkoa wa Arusha Cloud Gwandu, ametoa kauli hiyo wakati akizungumza katika zoezi la upandaji miti katika shule ya Sekondari Longido na Sekondari ya Tingatinga liliondeshwa na wanahabari kwa kushirikiana na wadau wa mzingira .

Gwandu amesema kuwa kutokana na ongezeko la tatizo la mabadiliko ya tabia ya nchi wanahabari wameamua kushiriki katika kurudisha uoto wa asili katika mazingira.

Alfred Mwakivike kutoka kampuni ya TGT wanaojihusisha na utunzaji wa mazingira amesema kuwa wilaya hiyo inakabiliwa na ukame kwa kiasi kikubwa hivyo zoezi la upandaji miti linapaswa kuwa endelevu.

Kwa upande wao wanafunzi wa Shule ya Sekondari Longido Grace Mkambala na Omari Shafi Omari wanafunzi wa kidato cha tano wamesema kuwa tayari wameanza juhudi za kutunza vitalu vya miti ikiwa ni pamoja na miti waliyopatiwa na wanahabari ambayo itasaidia kuboresha mazingira ya shule kuwa bora na yanayofaa kwa taaluma.

Wanahabari mkoani hapa wameshiriki katika zoezi la upandaji miti ambapo kwa mwaka huu na mwaka ujao wa 2017 wanatarajia kupanda miti laki moja katika shule za sekondari za kata ikiwa ni mchango wa wanahabari katika jamii inayowazunguka.