Jumamosi , 28th Jan , 2023

Jeshi la Polisi mkoani Arusha limeungana na watoto wanaoishi katika kituo cha kulelea yatima kijulikanacho kwa jina la Maasai Girls Rescue Center kilichopo wilaya ya Karatu kwa lengo la kuwaleta karibu watoto na jeshi hilo ili kupata taarifa za matukio ya ukatili wa kijinsia.

Baadhi ya Askari wa Jeshi la Polisi Arusha wakiwa na watoto yatima

Tukio hilo limefanyika leo Januari 28, 2023, Mkuu wa polisi wilaya ya Karatu Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SSP Radegunda Marandu, amesema jeshi hilo limetoa misaada mbalimbali kwa yatima hao ikiwa ni mkakati wa kuifanya jamii kuwa karibu nao.

SSP Marandu amebainisha kuwa pamoja na kuwa jeshi hilo linahusika na ulinzi wa raia na mali zao pia wanalo jukumu la kushirikiana na wananchi katika matukio  ya kijamii ikiwemo la kuonyesha upendo kwa yatima ambapo watakua huru kueleza changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo za ukatili.

Sambamba na hilo pia ametoa onyo kwa watu wachache ambao wana tabia ya kuwafanyia watoto vitendo vya ukatili kuacha mara moja kwani jeshi hilo lipo makini na litachukua hatua kali za kisheria dhidi yao.

Naye Bwana Elisante Loi, meneja wa kituo hicho amesema msadaa uliotolewa utawafanya watoto hao kujua kuwa polisi ni sehemu ya jamii hivyo watakua huru kueleza changamoto mbalimbali zinazowakabili kwa jeshi hilo bila kuogopa.