'Watoto wanaozaliwa wamepungua' - Waziri Ummy

Jumatano , 7th Aug , 2019

Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, amesema hatua ya kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa kwenye Shule za Msingi mkoani Tanga, haimaanishi kiwango cha wanawake kuzaa kimeongezeka.

Waziri Ummy Mwalimu ametoa kauli hiyo akiwa mkoani Tanga wakati wa utoaji wa msaada wa vitu mbalimbali, ikiwemo madawati katika Shule ya Msingi Kiruku iliyopo mkoani Tanga, ambapo amesema idadi kubwa ya watoto waliwakuwa hawaandikishwi shule kwasababu ya wazazi kukosa ada.

"Mimi nasimamia afya, sio kwamba wanawake wanazaa sana bali watoto wanaozaliwa wanapungua, ina maana watoto wengi walikuwa wanabaki nyumbani kwa sababu wazazi walikuwa hawana ada." amesema Ummy Mwalimu.

Waziri Ummy ameendelea kusema kuwa "kabla ya elimu bure watoto waliokuwa wanaandikishwa hapa Tanga walikuwa ni 8000, lakini baada ya elimu bure watoto wamefikia 10000, hatuna sababu ya kutokumshukuru Rais Magufuli"

Kwa sasa Serikali inatumia zaidi ya shilingi bilioni 23, katika kuhakikisha ina ratibu suala la elimu bure kuanzia ngazi ya Shule ya Msingi hadi Sekondari.