Alhamisi , 16th Mar , 2023

Wizara ya Afya imesema inafuatilia ugonjwa usiojulikana uliotokea mkoani Kagera wilaya ya Bukoba vijijini ambapo watu saba walipata dalili za homa, kutapika, kutokwa damu maeneo mbalimbali ya miili yao na Figo kushindwa kufanya kazi, ambapo watano wamefariki dunia na wawili wako hospitali.

Mganga Mkuu wa Serikali Profesa Tumaini Nagu,

Wizara ya imesema inafuatilia ugonjwa usiojulikana uliotokea mkoani Kagera na kuua watu watano baada ya watu saba kupata dalili za homa, kutapika, kutokwa damu maeneo mbalimbali ya miili yao na Figo kushindwa kufanya kazi, ambapo wawili wako hospitali.

Taarifa hiyo imetolewa leo Machi 16, 2023, na Mganga Mkuu wa Serikali Profesa Tumaini Nagu, na kusema Ugonjwa huo usiojulikana umetokea wilaya ya Bukoba vijijini katika vijiji vya Bulinda na Butayaibega, ambapo inasadikiwa watu hao saba walipata dalili hizo za homa.

"Serikali imechukua hatua za kudhibiti ugonjwa huo ili usisambae kwa kuchukua sampuli kutoka kwa wagonjwa na waliofariki ili kubaini chanzo cha ugonjwa huo na ufuatiliaji wa watu wenye viashiria vya ugonjwa kwenye jamii," amesema Profesa Nagu.

Aidha Profesa Nagu ameongeza, "Pia dawa, vifaa na vifaa tiba muhimu vipo katika vituo vya kutolea huduma za afya mkoani Kagera na wagonjwa wanaendelea na matibabu, na elimu ya afya inaendelea kutolewa kwa jamii mkoani Kagera ili kuchukua tahadhari,"- Profesa Tumaini Nagu, Mganga Mkuu wa Serikali

Katika hatua nyingine Wizara ya Afya imewatoa hofu Watanzania kuhusu ugonjwa huo na kushauri, "Mtu yeyote mwenye dalili za homa, kutapika, kuharisha, kutoka damu na mwili kuishiwa nguvu anashauriwa kuwa kituo cha kutolea huduma za afya, kuepuka kumgusa mgonjwa au majimaji ya mwili, mate, machozi, damu, mkojo na kinyesi kitokacho kwa mgonjwa au yeyote mwenye dalili hizo,".