Jumapili , 13th Oct , 2019

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ametoa sababu zilizopelekea vitalu vingi vya uwindaji wa wanyamapori nchini kukosa wawekezaji na hata baadhi ya wawekezaji waliokuwa wanamiliki baadhi ya vitalu hivyo kulazimika kuvirudisha Serikalini.

Naibu Waziri Kanyasu amemsema sababu kubwa iliyopelekea tatizo hilo ni mifugo kuingizwa ndani ya hifadhi na kuwafanya wanyamapori wengi kuhama.

Kanyasu amesema Wanyamapori hulazimika kuhama maeneo yaliyovamiwa na ng'ombe kwa sababu hushindwa kuvumilia harufu inayotoka kwa ng'ombe, kufutia madawa ambayo hutumika kuoshea wanyama hao.

Amesema kufuatia hali hiyo vitalu vingi vimekuwa havina wanyamapori na badala yake, vimekuwa na ng'ombe hali inayosababisha wawakezaji wengi kulazimika kuvirudisha vitalu hivyo, kwa sababu hawajavichukua kutoka Serikalini kwa ajili ya kuwinda ng'ombe.

Akizungumza katika Pori la Akiba la Moyowosi-Kigosi na watumishi  wa kituo cha Ipole Kaskazini mwa pori hilo kwa upande wa Geita, Waziri Kanyasu amewataka watumishi hao kuimarisha ulinzi kwa kufanya doria madhubuti, ili kuzuia wafugaji wasiweze kuingiza ng'ombe katika pori hilo

Ameyataja Mapori ya Akiba yaliyoathirika na mifugo na kufanya wawekezaji kurudisha vitalu hivyo kwa wingi  kuwa ni Pori la Ugalla pamoja Moyowosi mkoani Kigosi.

Amesema kufikia mwezi Juni mwaka huu, jumla ya vitalu vipatavyo 60 kutoka mapori ya akiba mbalimbali vilikuwa vimerudishwa Serikalini kutoka kwa wawekezaji.