Wazee wa Manispaa ya Singida wamelaani madada poa wanaofanya biashara haramu ya kujiuza katika eneo lililopo karibu na shule ya msingi na misikiti.
Akizungumza kwa niyaba ya wazee hao Sheikh Mohammed Ihucha katika kikao maalum kilichoitishwa na mbunge wa Jimbo la Singida mhe. Yagi Kiaratu ili kuzungumza na wazee wa jimbo hilo, amesema kuwa madada poa hao wamekuwa wakisababisha hata maadili ya watoto kuharibika kwakuwa wanafanya biashara hiyo karibu na shule ya Msingi Mughanga na wanaanza saa kumi na moja jioni bila kujali kuwa ni karibu na shule na msikiti.
Amesema kuwa watu hao wanafanya biashara hiyo haramu na kwasasa imekuwa kero kubwa huku akihoji kama ni biashara je wanalipa kodi kwa nani?
Wameiomba Serikali kukomesha tabia hiyo kwa kuwa imezidi kukithiri katika eneo hilo ambapo EATV ilitembelea eneo hilo na kukuta makundi ya vijana wakiwa ndio wateja wakubwa wa madada poa hao hali ambayo inahatarisha usalama wa afya zao kwa kupata magonjwa yatokanayo na ngono.
Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Singida amesema kuwa suala hilo litapelekwa kwenye vikao vya baraza la madiwani ili kukomesha tabia hiyo chafu katika jamii huku ikielezwa kuwa wengi wao wanaofanya biashara hiyo sio wenyeji wa Singida wakiwa wametoka mikoa mbalimbali.
Mbunge wa jimbo hilo Yagi Kiaratu, amefanya kikao na wazee ili kuwasikiliza na kupata mwanga wa kutatua baadhi ya kero zao huku akikemea tabia ya wauguzi na madaktari kuwasumbua wazee wanaokwenda hospitali kupata matibabu.

